 |
TUFUNDISHE Kigazeti
Igizo Poa
Lenye Mwanga |
Njia ya Kwenda Mbinguni
Wachezaji:
Fred (kijana)
Charles (kijana)
Mama Wile (mwanamke) Vifaa:
Esta (msichana) Ramani au karatasi
Mzee (mwanaume) Biblia 2
Fred na Charles wataingia kwa pamoja)
FRED: (Atamwangalia Charles machoni.) Je, wewe utafanya nini?
CHARLES: Kuhusu nini?
FRED: Mchungaji Peter aliniuliza nilipomwambia kuwa nilipenda
mahubiri yake Jumapili iliyopita. Aliniangalia machoni (Fred
amwangalie Charles machoni tena) kisha akasema, “Je, sasa wewe
utafanya nini, Fred?!”
CHARLES: AAH! Ukamwambiaje?
FRED: Nilitulia sekunde chache kisha nikasema nadhani
nitafikiria vizuri swali lake, kwa sababu sikuweza kujibu lolote.
CHARLES: Mchungaji Peter alitufundisha kuwa watu wengi
wanatupita na hawaijui njia ya kwenda mbinguni na ni wajibu wetu
sisi kuwaambia. Je, wewe utafanya?
FRED: Sio mimi peke yangu, Charles. Wewe pia, si ndiyo?
CHARLES: Najua, kama kweli tunajali tungeenda kwa pamoja
kuwaambia habari njema na kuwaonyesha njia ya mbinguni!
FRED: Haya sasa, tuanze kuongea na watu wanaopita hapa. Mmoja
akiwa anaongea na mtu, mwingine awe kwenye maombi kwa ajili yake.
Sawa, Charles?
CHARLES: Sawa, ila wewe anza kwanza kuongea, Fred. Nina
wasiwasi bado.
FRED: Uanze kuongea na Mungu, Charles, nasikia sauti ya mtu
akitembea karibu. (Mama Wile aingie.) Shikamoo, Mama.
MAMA WILE: Marahaba. Hujambo?
FRED: Sijambo. Je, unaijua njia ya kwenda mbinguni?
MAMA WILE: Ndiyo, naijua. Je, unataka nikuonyeshe njia hiyo?
FRED: Hapana, mama. Naijua pia. Nilitaka nihakikishe tu kama
unaijua njia hiyo.
MAMA WILE: Vizuri sana! Mungu akubariki. Umenibariki sana!
Nitakuombea. Naenda sasa. Kwa heri.
(Kisha Mama Wile atoke.)
CHARLES: Huu ni mwanzo mzuri. (Esta aingie.) He! Esta
huyooooo anakuja, mimi siwezi kuongea naye.
FRED: Lazima tumwambie. Kila mtu ni lazima ajue.
FRED: Vipi, Esta. Habari? Nisubiri kidogo.
ESTA: Bwana, mi nina haraka.
FRED: Unaijua njia ya mbinguni?
ESTA: Kweli unamaanisha usemacho?
FRED: Ndiyo, nataka kujua kwa hakika kama unaijua njia hiyo.
Maana Yesu alikufa kwa ajili yako na ukitubu na kumwamini
atakusamehe na utaokoka. Yesu pekee ndiye njia ya mbinguni.
ESTA: Vizuri.....Nitafikiria na nitakuona baadae.
(Esta atoke.)
FRED: .....Ona, Mzee anakuja sasa. Ni zamu yako, Charles.
(Mzee aingie.)
CHARLES: Shikamoo, Mzee.
MZEE: Marahaba.
CHARLES: Samahani, Mzee. Je, unaijua njia ya mbinguni?
MZEE: Kitu gani hicho? Vipi, unacheza? Unanitania sasa?!
CHARLES: Hapana, Mzee, kama hauijui tunataka kukuonyesha.
MZEE: Sikiliza kijana, we umeshawahi kwenda huko?
CHARLES: Hapana....ila......
MZEE: Sasa wewe utaijuaje njia? Haya, hebu niambie unaijua
njia ya Iringa?
CHARLES: Hapana....
MZEE: Kwa hiyo huijui njia....Sikilizeni vijana. Watu
wanawaambia kuwa kuna mbingu na njia ya kufuata....halafu mnaamini....wakati
hamjawahi kufika mbinguni wala kumwona mtu aliyetoka huko.
FRED: Hiyo si kweli, mzee. Yesu alitoka huko na Yeye ali......!
MZEE: Alifanya nini?
CHARLES: Unaweza kunisubiri? Nakuja sasa hivi.
(Charles atoke.)
MZEE: Haya nakusubiri. Fanya haraka.
(Charles aingie na ramani.)
CHARLES: Mzee nimerudi! Hii ni ramani ya Tanzania. Sijui hata
aliyeichora ila ninaamini ukianzia hapa na kufuata barabara hii
utafika Iringa.
MZEE: Ninakubali. Ila, je, unawezaje kunihakikishia?
CHARLES: Pamoja na sijawahi kufika Iringa, ila naweza
kukuonyesha njia sababu kuna mtu aliyewahi kufika huko ametuelekeza.
MZEE: Hivyo unawezaje kwenda mbinguni?
CHARLES: Yesu tayari alishatoka mbinguni na maelekezo ya njia
ya kwenda mbinguni yapo kwenye Biblia. Na kama tuliweza kuiamini
ramani iliyotengenezwa na mtu, je, si zaidi sana kuiamini Biblia
iliyo na maneno ya Mungu?
MZEE: .....Unajua, kijana, kuna kitu hapa! .....Sawa....niko
tayari kuwasikiliza Fungueni Biblia na mnielekeze njia ya mbinguni.
(Kisha wote watoke.)
Maelezo ya Vifaa:
Fred na Charles wabebe Biblia zao.
Karatasi ya ramani iwe tayari nyuma kwa Charles kuchukua
atakapoihitaji.
TUFUNDISHE Aug/Sept
2007 Vol. 1 No. 2
Back to index
|